Shirika la MUHURI ladai fidia


Shirika la MUHURI ladai fidia

Aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga amesema alipokea kwa mshangao taarifa ya kufungwa kwa akaunti za benki ya shirika la kutetea haki za kibinaadam la MUHURI kwa madai ya kuhusishwa na shughuli za kuwafadhili magaidi.

Akitoa ushahidi mbele ya jaji Dora Chepkwony, Mutunga, ambaye ni mmoja wa mashahidi kwenye kesi iliyowasilishwa na shirika la MUHURI kutaka fidia kwa madai ya kuchafuliwa jina, amesema ni dhahiri kuwa hakuna wafadhili ambao wangejitokeza kutoa msaada kwa shirika lolote linalohusishwa na suala la ugaidi hali ambayo ingeathiri shughuli zake.

Aidha Mutunga amesema kwamba alikuwa miongoni wa waanzilishi wa shirika hilo takriban miaka 21 iliyopita na kushikilia kuwa anafahamu shirika hilo na viongozi wake kama watu wanaotii sheria, na hivyo haamini kwamba wangeweza kufadhili au kushirikiana na magaidi katika shughuli zao.

Akitotoa ushahidi wake mwenyekiti wa shirika hilo Khelef Khalifa amesema kwamba kwa muda wa miezi minane ambayo akaunti zao zilifungwa, shughuli zote zililemazwa kwani hawakuwa hata na hela za kuwalipa wafanyikazi wao.

Shirika la MUHURI lilikuwa miongoni mwa mashirika 85 yaliyoamriwa kufungwa na Inspekta Jenerali wa polisi Aprili mwaka wa 2015 kwa madai ya kufadhili ugaidi.

Hata hivyo shirika hilo liliwasilisha kesi mahakamani iliopelekea kufunguliwa kwa akaunti zake mnamo Novemba miezi minane baadaye, hali iliyopeleka wasimamizi kuwasilisha kesi mahakamani kudai fidia.

For Citizen TV updates
Join @citizentvke Telegram channelVideo Of The Day: CBK\'s guidelines on how to return 1000 notes

Avatar
Story By Babu Abdalla
More by this author