WASILWA: Namkumbuka Waweru Mburu


waweru mburu
Radio Citizen veteran broadcaster, the late Waweru Mburu. Photo: File

Ningependa kumtabarukia makala haya marehemu, Peter Waweru Mburu.  Mwanafilosofia mmoja alisema kuwa, na nina mnukuu: “Kila mmoja wetu ni muigizaji, ulimwengu ndio ukumbi wa kuigiza na Mwenyezi Mungu ndiye mwelekezi wa mchezo wenyewe.” Hapa ulimwenguni sote tunaigiza, ulimwenguni ndipo tunapoigizia tamthilia hii inayoitwa maisha na kwamba Mungu Muumba ndiye anayetuelekeza kwa sababu ndiye chanzo cha mwanadamu.

Kwenye mchezo huu wa maisha zipo siku tatu kuu za maisha ya mwanadamu, kuzaliwa, kuoa au kuolea na kisha kuaga dunia. Hadi sasa ningali nadinda kukubali kuwa mwenzetu ametuaga, kila ninavyozidi kutafakari, ndivyo navyozidi kudhani kwamba mwendazake amelala tu, na kwa kipindi kifupi ataamka na kuendelea kuchangia katika jamii, lakini ukweli mchungu ambao hadi sasa nimekataa asilani kuuafiki ni kuwa, mtangazaji mwenzangu, baba, kaka, hatarudi daima dawamu.

Ni ukweli mchungu ambao unaghasi, kuchosha na kuchusha moyo wangu na mashabik wa makala yake. Peter Waweru Mburu maarufu kwenye makala Yaliyotendeka hayuko nasi tena. Ama kwa hakika mchango wa mzalendo huyu, mwana wa Kenya, kwenye masuala ya jamii, na tasnia nzima ya uanahabari hauwezi ukasahaulika. Utasahaulika vipi na makala hayo yalikuwa yanapigania haki na usawa kati ya matabaka yaliyonavyo na yasiyo navyo.

Makala ambayo yalimkweza mnyonge na kumpa sauti kwenye ulimwengu uliosheheni papa na mamba. Yatasahaulika vipi na Makala hayo ndio yamezaa makala ya Ninapobanwa kwenye Radio Citizen. Ni sauti iliyorindima ndani na nje ya mipaka ya Kenya. Sauti jasiri, shupavu ambayo haikuwa na kitetemeshi. Ni sauti ambayo kila mara ingesikika hewani taifa zima lingesimama na kusikiza mzalendo huyu alikuwa anasema nini. Viongozi wakuu na walala hoi wangetekwa na makala ya Yaliyotendekea.

Sauti yake ilichinja na kutakasa jamii kwa viwango sawa, ikivunja mihimili ya uovu katika jamii. Wafisadi hawakusazwa. Saa mbili usiku juu ya alama na marejeo yake saa moja kasorobo asubuhi kwenye ukumbi huu.

Kwenye makala moja bunge lilitenga awamu nzima ya kujadili makala yake. Kwamba wabunge waliguswa haikuwa mjadala. Wabunge walionekana kujiongezea mishahara kila mara, suala ambalo halikumuudhi tu Mburu bali wakenya wanyonge. Injili yake Mburu ililenga kungazia uozo wa jamii. Suala la maadili ya viongozi na jamii pana akilipa uzito uliostahili.

Hakujali mirengo ambayo mmoja alikuwa anaegemea kwenye siasa. Hapo alipendwa na wengi na pia kuchukiwa na wengi. Alipendwa kwa sababu alitetea jamii ya mlala hoi na kuchukiwa na walala heri kwa sababu hakuwapaka mafuta. Aliwafahamisha ukweli japo ulikuwa mchungu. Kwamba injili yake ilipasua na kukata kuwili. Kwenye kituo hiki nadata, nahisi ujumnyosis kama anayosema mwandishi Said A. Mohammed hisia za ujuto ujuto, ubaridi ubaridi na mnyengereko na machozi.

Nauliza maana kuntu ya maisha, Mbona mwanadamu atambe na kutaratamba maishani akazoa atakayowezeshwa kuzoa kisha mwisho wake ukawa kama barafu iliyoyeyuka? Mbona hili ua lichanue asubuhi na kutoa harufu nzuri ya kuvutia kisha jua linapofika utosini likanyauka kana kwamba halikuwahi kuwa na uhai. Nyota ya Waweru imefifia ila falsafa zake na mtazamo wake utasalia nasi daima dawamu. Ninapobanwa inahisi kwamba mbegu alizopanda Mburu, zimezaa baadhi ya wana ambao siku moja watakuwa na azma ya kujitosa kwenye nyanja hii ya habari.

Wengine ni wanahabari japo hawajapata kiambajengo cha kujieleza, Ninapobanwa inawafahamisha kuwa wasife moyo, kwamba ipo siku nyota zao zitang’aa na kupasua mawimbi ya radio na televisheni na kuendeleza falsafa za Mburu.

Kuondoka kwa Mburu kunahalisi msemo kuwa ivumayo siku zote haidumu na kwamba mshale mzuri haukai ziakani. Kuvuma kwa zaidi ya mwongo mmoja kwenye radio kila siku, sio kazi lelemama. Ametufunza kuwa na msimamo thabiti, ametufunza kuwa kwenye mrengo wa haki na uadilifu. Ametufunza kujitolea kwa dhati kwa kila kitu ambacho tunafanya.

Badala ya kulalama, ametufanza kufanya angaa japo jambo dogo ili kuleta mabadiliko. Historia ya taifa siku moja itakapokuwa inaandikwa, Mburu atatajwa kuwa mmoja wa sauti ambazo zilichangia ukombozi wa pili. Sauti yake ilikemea maovu kwenye utawala wa rais mstaafu Daniel Arap Moi kwa mapana na marefu yake. Sauti yake ilileta mwamko na uzinduzi mpya ambao wakenya hawakuwa wamewahi kushuhudia kwenye utawala wa chama kimoja cha KANU.

Kila mara akiongozwa na falsafa za usawa, haki na demokrasia. Zawadi nzuri ambayo jamii aliyoipigania kwa hali na mali inaweza ikamkabidhi mzalendo huyu, ni kuendeleza moyo wa taifa yenye haki kwa kila mmoja wetu bila ya kuzingatia kabila, rangi wala dini. Kinachonipiga pute kama si bumbuwazi ni kuwa Mburu ametangulia mbele za haki na wingi wa busara, insafu na mlahaka mzuri pamoja na amali zote njema ambazo, familia na jamii pana ilikuwa ingali inahitaji kuteka kutoka kwake.

Baada ya yote kusemwa, jambo moja ni yakini kama kiza na nuru. Kwamba kazi ya mwenyezi Mungu wala haina doa au toa, makosa wala taksiri, apangaye Yeye lazima yatimie.

Simbolezi kuondoka kwa Mburu mapema miongoni mwetu bali, nafurahia msingi bora alioujenga na kiambajengo hiki cha kutetea maslahi ya mkenya mzalendo. Ninafurahi nyakati nyingi ambazo Mburu alitekeleza wajibu wake kwa ukamilifu na utaalamu wa hali ya juu. Ninashikilia kuwa mbegu ambazo ameacha zitachanua siku moja na kwamba hatutakuwa tukijitambulisha kwa misingi ya kabila, dini wala rangi.

Dhulma dhidi ya wanyonge katika jamii itakuwa jambo la historia. Mburu alikuwa na silaha tatu alizotomia kwa ufasaha mkubwa kwa zaidi ya mwongo mmoja na zaidi alipohudumu kwenye kampuni ya Royal Media services- Sauti yake iliyokuwa na madende kila mara akiivuta ikipasua mawimbi, mashariki hadi kusini, kaskazini na magharibi. Kalamu aliyotumia kuandika makala hayo na umilisi wa lugha ya Kiswahili aliyotumia kupitisha ujumbe wake.

Ungemsikiza jinsi alivyocheza na maneno akitumia misemo, methali na wakati mwingine kinaya. Peter Waweru Mburu alizaliwa mwaka 1962, Alisomea shule ya upili ya Makuyu kati ya mwaka 1979 na mwaka 1983. Baadaye alijiunga na shule ya upili ya Emusire kati ya mwaka 1984 hadi mwaka 1985. Alijiunga na chuo kikuu cha Nairobi kati ya mwaka 2006 na mwaka 2009 kwa shahada ya sana katika masuala ya uanahabari.

Kati ya mwaka 2010 na mwaka 2012 alifuzu kwa shahada ya uzamili katika masuala ya habari na mawasiliano kwenye chuo hicho. Alikuwa mwalimu wa shule ya upili ya Makuyu kati ya mwaka 1986 hadi mwaka 1997 kabla ya kuogelea kwenye bahari ya uandishi wa habari. Alijiunga na kituo cha Royal Media Services mwaka 1999 hadi kifo chake ambapo alikuwa akisimamia idhaa ya kiswhaili. Alikuwa anaugua saratani ya tumbo. Ameacha mjane na watoto watatu.

Kwa kituo hicho nahitimisha makala kwa kauli ya mwanafilosofia mmoja kuwa, “ maisha alimuuliza kifo, mbona watu wananipenda na wewe unachukiwa. Kifo alijibu, kwa sababu maisha yako ni ya uwongo nami ni ukweli mchungu.”  Na huo ndio ukweli mchungu.

Shisia Wasilwa ni mhariri wa Royal Media Services Ltd

For Citizen TV updates
Join @citizentvke Telegram channelVideo Of The Day: Former sports CS Hassan Wario convicted over Rio games scam

Avatar
Story By Shisia Wasilwa
More by this author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *