WASILWA: Ukabila nyama gani?

WASILWA: Ukabila nyama gani?

Ukabila ni ugonjwa mbaya zaidi ya saratani, mtu mmoja alinukuliwa akisema. Ukabila umeyaacha mataifa mengi barani Afrika bila ya ustawi badala yake damu ya watu imechora barabara za mataifa hayo. Mataifa kama vile Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na hata Rwanda ni mifano ya mataifa ambayo yameshuhudia umwagikaji wa damu na kuachwa na michibuko na mikwaruzo ya ukabila.

Kwamba unapoona viongozi wakiendekeza ukabila kwenye asasi za elimu ya juu, fahamu kuwa pana tatizo kubwa zaidi. Iwapo viongozi watajificha kwenye mwavuli wa kabila na koo zao, je, itakuaje kwa mwananchi wa kawaida, ambaye mara nyingi hajapata elimu?  Taasisi zote za umma humu nchini ni za Wakenya. Ni za wakenya kwa misingi kuwa hakuna kabila ambalo linamiliki taasisi yoyote. Kwa mujibu wa katiba inayolinda nchi, Mkenya kutoka pembe yoyote ya taifa ana uhuru na haki ya kuhudumu kwenye asasi yoyote ya taifa, haijalishi rangi kabila, ukoo wala dini yake.

Kwamba asasi zile zinaendeshwa na hela zako na zangu kwa maana kuwa ni pesa za mtoza ushuru. Ikiwa huo ndio ukweli mchungu, inapoteza maana mmoja akijitokeza na kutangaza mchana wa jua kuwa Fulani hafai kuhudumu ama kuongoza taasisi ile kwa misingi kuwa kabila lake si la wenyeji. Je, tunapokaribia uchaguzi mkuu, taswira kama iliyoshuhudiwa katika chuo kikuu cha Moi, inaonyesha nini? Je, vyuo vya umma vilivyojikita katika maeneo mbali mbali ya taifa havifai kuongozwa na watu kutoka maeneo mengine ya taifa? Siasa za ukabila zitaisha humu nchini?

Ni tamthlia ambayo wakenya wamezoea kushuhudia. Mazingira ambamo wahusika wanachezea tamthiliya yenyewe ni Uasin Gishu. Wahusika wakuu kwenye tamthilia hiyo ni Magavana wa Uasin- Gishu Jackson Mandagor na Alex Tolgos wa Elgeyo Marakwet. Wahusika wadogo ni wabunge Oscar Sudi wa Kapasaret, Silas Tiren wa Moiben, James Bett wa Keses, na spika wa bunge la Uasin Gishu Isaack Terer Marakwet. Wahusika hao wanaongoza jamii yao kupinga uteuzi wa kaimu chansela wa chuo kikuu cha Moi profesa Laban Ayiro.

Hatua hiyo haivunji tu matumaini ya mshikamano wa moja taifa bali unatisha kutawanya na kuvuruga amani iliyopo maanake inajiri wakati wakenya wanajiribu kusahau yaliyotokea mwaka 2007.  Kwamba ukabila ulichangia pakubwa wakenya walipouana wenyewe kwa wenyewe. Leo ukitembea maneo yaliyoathirka utagundua kuwa baadhi ya watu waliopoteza makazi hawajarejea. Kitendo cha viongozi hao kinadhihirisha kuwa wao si marafiki wa taifa bali ni maadui wakubwa ambao wanastahili kukemewa na kukashifiwa.

Kaparo anastahili kuwachukulia hatua za kisheria. Kitendo chao ni sawa na kutia kuni kwenye kuni zilizo na petroli. Kitendo chao kinadhalilisha hadhi ya kuwa kiongozi nchini. Hayo yanafanyika licha kuwa kifungu cha sita cha katiba kinaelezea sifa za kiongozi. Je, mustakabala wa taifa ni upi na viongozi kama hao?

Waziri wa elimu daktari Fred Matiangi alimchagua profesa Laban Ayiro kuwa kaimu naibu wa chansela kwa kuzingatia kanuni za chuo kikuu, hata hivyo viongozi wa eneo hilo wanaona kuwa hatua ya matiangi inadhalilisha mtu wa jamii yao. Natarajia kuwa uteuzi wa waziri Matiangi utasalia. Tunavyomjua waziri ni kuwa si mtu wa kutishwa na kwamba anafahamu wajibu wake. Ila wao wanamtaka Profesa Isaack Kosgei badala yake.

Wanasema kuwa mtu wao aliongoza kwenye mahojiano na kwamba waziri alikosea kumchagua profesa Ayiro. Profesa Ayiro ambaye kwa sasa ni kaimu naibu wa chansela katika chuo hicho alikuwa naibu wa chansela wa mipango. Viongozi hao sasa wanatisha kusambaratisha sherehe ya wanafunzi kufuzu katika chuo kikuu cha moi mjini Eldoret iliyoratibiwa kufanyika siku ya Alhamisi na Ijumaa iwapo profesa Isaac Kosgey hatateuliwa kuwa chansela wa chuo hicho. viongozi hao wanadai kwamba kosgey ndiye anayestahili  kumrithi profesa Richard Mibey ambaye muda wake umekamilika.

Kama huo si uwendawazimu tuiteje. Hilo linafanyika kwenye taifa ambalo lina zaidi ya makabila 40. Kinaya ni kuwa hawa ndio viongozi ambao tunawategemea kutufikisha kanani. Watufikishe kwenye ndoto za taifa mwaka 2030. Ninapobanwa inashikilia kuwa mawazo kama yale hayatatufikisha mahali.

Kwamba baadhi ya mambo yanayoua na kudemaza viwango vyetu vya elimu ni ukabila kwenye asasi zetu za juu za elimu. Kwamba viongozi wa makabila hutumia nafasi zao kusukuma ajenda za makabila yao. Hatua ambazo kwa kweli zilipitwa na wakati. Wakenya wanawakumbusha  viongozi wa kikabila kuwa huu ni ulimwengu wa sasa, hii sio Kenya ya jana hii ni Kenya ya leo. Kenya ya leo imebadilika, vijana hawajitambulishi kwa misingi ya makabila yao. Wanajitabulisha kwa uwezo na vipaji vyao.

Ripoti ya Tume ya kitaifa ya Uwiano na maridhiano inachora taswira ya kuhofisha. Kwamba asilimia 80 ya taasisi za umma zimekiuka sheria ya uteuzi. Sheria inaeleza kuwa haistahili kwa jamii moja kuwa na zaidi ya asilimia 30 ya ajira kwenye vyuo vikuu.  Mapema mwaka huu, viongozi wa makabila walivamia chuo kikuu cha Eldoret na kujaribu kumtimua Teresia Akenga, ambaye si mzawa wa eneo hilo kuwa alichaguliwa kuwa naibu wa chansela wa chuo hicho. Waziri wa Elimu wakati huo Jacob Kaimenyi alikaa ngumu, lau Akenga angetimuliwa mchana wa Mungu. Mbona tunarejesha nyuma taifa kwa ujinga sampuli hii.

Yafaa tuangalie jinsi mmoja alivyohitimu pamoja na uzoefu wake badala ya kuangalia kabila la mtu. Mbona tunapenda kukuza sana ukabila licha ya kufahamu madhara yake. Iwapo asasi zetu za elimu ya juu zitageuzwa kuwa madhabahu na vyungu vya ukabila, lini tutapata wazalendo wasiofahamu msamiatu wa ukabila? Ripoti ya Kaparo inaonyesha kuwa makabila matano nchini yamesheheni kwenye asasi za elimu ya juu.  Kwamba katika chuo kikuu cha Masinde Muliro asilimia 93 ya wafanyikazi ni wa jamii inayopatikana kule. Asilimia 90 ya wafanyikazi wa chuo kikuu cha Moi ni ya watu wa jamii ya watu wa kule.

Asilimia 97 ya wafanyikazi wa chuo kikuu cha Egerton ni wenyeji, katika chuo kikuu cha Jomo Kenyatta asilimia 96 ya wafanyikazi ni wenyeji. Hali sio tofauti katika vyuo vikuu vya Nairobi na Kenyatta ambapo asilimia 82 ya nafasi za kazi zinamilikiwa na watu wa makabila makuu nchini. Hayo ndio masaibu ya vyuo vyetu vikuu. Taswira inaharibiwa na hali kuwa mtoto anapozaliwa eneo Fulani husomea eneo lile lile-shule ya msingi na upili. Chuo kikuu akasomea pale pale. Mtoto Yule anakosa mtagusano na jamii pana.

Akafunga pingu za maisha katika eneo lile na mwenzake wa jamii hiyo hiyo. Mtu kama Yule ni hatari kwa jamii, kwa sababu mawazo yake ni finyu na ndogo kwa maendeleo ya taifa. Iwapo, taifa litashinda hivi vita vya ukabila, ni muhimu mosi kwa viongozi wa makabila kupigwa marufuku. Viongozi kama wale hawafai kuwania nyadhfa zozote zile. Mfumo wa utawala wa ugatuzi unastahili pia kutekelezwa kwa wanafunzi kiasi kuwa mwanafunzi aliyezaliwa Kakamega akihitumi kujiunga na shule ya upili anapelekwa eneo la kati ya Kenya.

Hivyo mwanafunzi Yule atakuwa anapanuliwa mawazo na mtazamo wake.  Kwa kituo hicho nakamilisha na usemi wa mwanfilosofia mmoja aliyesema kuwa gharama ya elimu ni unyenyekevu. Unapokutana na mtu mwenye kiburi akizungumza anajipiga kifua kwake wengine ni watu wadogo sana, basi fahamu kuwa mtu Yule hajaelimika.

Want to send us a story? SMS to 25170 or WhatsApp 0743570000 or Submit on Citizen Digital or email wananchi@royalmedia.co.ke

Leave a Comment

Comments

No comments yet.

latest stories